Zaburi 113 (NEN)
Zaburi 113
Kumsifu Bwana kwa wema wake
1 Msifuni Bwana.113:1 Msifuni Bwana kwa Kiebrania ni Hallelu Yah; pia 113:9.
Enyi watumishi wa Bwana msifuni,
lisifuni jina la Bwana.
2 Jina la Bwana na lisifiwe,
sasa na hata milele.
3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake,
jina la Bwana linapaswa kusifiwa.
4 Bwana ametukuka juu ya mataifa yote,
utukufu wake juu ya mbingu.
5 Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu,
Yule aliyeketi kwenye kiti cha enzi huko juu,
6 ambaye huinama atazame chini
aone mbingu na nchi?
7 Huwainua maskini kutoka mavumbini,
na kuwanyanyua wahitaji
kutoka lundo la majivu,
8 huwaketisha pamoja na wakuu,
pamoja na wakuu wa watu wake.
9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake,
akiwa mama watoto mwenye furaha.
Msifuni Bwana.