Zaburi 124 (NEN)
Zaburi 124
Shukrani kwa ukombozi wa Israeli
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Kama Bwana hangekuwa upande wetu;
Israeli na aseme sasa:
2kama Bwana hangekuwa upande wetu,
watu walipotushambulia,
3 hasira yao ilipowaka dhidi yetu,
wangetumeza tukiwa hai,
4 mafuriko yangegharikisha,
maji mengi yangetufunika,
5maji yaendayo kasi
yangetuchukua.
6Ahimidiwe Bwana,
ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
7 Tumeponyoka kama ndege
kutoka mtego wa mwindaji;
mtego umevunjika,
nasi tumeokoka.
8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.