Zaburi 7 (NEN)
Zaburi 7
Sala ya mtu anayedhulumiwa
Ombolezo la Daudi kwa Bwana kwa sababu ya Kushi, Mbenyamini.
1 Ee Bwana, Mungu wangu, ninakukimbilia wewe,
uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,
2 la sivyo watanirarua kama simba
na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa.
3 Ee Bwana, Mungu wangu, kama nimetenda haya
na kuna hatia mikononi mwangu,
4au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami,
au nimemnyangʼanya adui yangu pasipo sababu,
5basi adui anifuatie na kunipata,
auponde uhai wangu ardhini
na kunilaza mavumbini.
6 Amka kwa hasira yako, Ee Bwana,
inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu.
Amka, Mungu wangu, uamue haki.
7 Kusanyiko la watu na likuzunguke.
Watawale kutoka juu.
8 Bwana na awahukumu makabila ya watu.
Nihukumu Ee Bwana,
kwa kadiri ya haki yangu,
kwa kadiri ya uadilifu wangu,
Ewe Uliye Juu Sana.
9 Ee Mungu mwenye haki,
uchunguzaye mawazo na mioyo,
komesha ghasia za waovu
na ufanye wenye haki waishi kwa amani.
10 Ngao yangu ni Mungu Aliye Juu Sana,
anayewaokoa wanyofu wa moyo.
11 Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Mungu anayeghadhibika kila siku.
12 Mtu asipotubu,
Mungu ataunoa upanga wake,
ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.
13 Ameandaa silaha zake kali,
ameweka tayari mishale yake ya moto.
14 Yeye aliye na mimba ya uovu
na anayechukua mimba ya ghasia huzaa uongo.
15 Yeye anayechimba shimo na kulifukua
hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe.
16 Ghasia anazozianzisha humrudia mwenyewe,
ukatili wake humrudia kichwani.
17 Nitamshukuru Bwana kwa ajili ya haki yake,
na nitaliimbia sifa jina la Bwana Aliye Juu Sana.